MKAKATI WA WFP NA NFRA KUMALIZA KILIO CHA WAKULIMA


pic+kilimo
DAR ES SALAAM
SEKTA ya Kilimo nchini imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda.
Sekta hii ina umuhimu wa kipekee katika mustakabali wa maisha ya watanzania wengi kiuchumi na ushiriki wao katika ujenzi wa uchumi tarajiwa wa viwanda. Sekta hiyo imeendelea kuimarika na hivyo kuchangia asilimia 30.1 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 29.2 kwa mwaka 2016.
Taarifa ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, inaonyesha kuwa tathmini ya uzalishaji wa mazao ya nafaka ikiwemo mahindi, mpunga, uwele na mtama ambayo ndiyo kipimo kikuu cha hali ya upatikanaji wa chakula nchini ulifikia tani 15,900,864 kwa msimu wa mwaka 2016/17.
Aidha upatikanaji wa chakula nchini ukilinganishwa na mahitaji umeendelea kuwa imara ambapo, mahitaji ya chakula kwa mwaka 2017/18 yalikuwa tani 13,300,034 kati ya hizo, mahitaji ya nafaka ni tani 8,457,558 na mazao yasiyo ya nafaka ni tani 4,842,476. 
Inaelezwa kuwa asilimia 20 mpaka 40 ya mazao hasa mahindi yanayovunwa na wakulima hupotea tangu yanapovunwa, kusafirishwa na kuhifadhiwa katika maghala  pamoja na matumizi ya kemikali ambazo huwa na madhara kwa mazao.
Ripoti ya Mapitio ya Kiuchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) yam waka 2017 inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya mazao  yanayohifadhiwa katika maghala ya watu binafsi na yale ya serikali hupungua thamani kwa sababu mbalimbali ikiwemo kushambuliwa na wadudu. 
Aidha ripoti hiyo inaeleza kuwa kati ya tani 74,826 za mahindi zilizokuwepo katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), tani 106 zilipotea kutokana na vumbi la viuatirifu na kuharibika kwa mahindi hayo kulitokana na kukaa kwa muda mrefu.
Huo ni mfano mmoja wa chakula kinachopotea katika maghala ya wakulima kwa sababu ya mbinu hafifu za utunzaji wa mazao kabla hayajauzwa na kutumika, hatua inayosababisha wakulima wengi kutumia nguvu kubwa wakati wa kulima na mwishoni kukosa kipato cha uhakika wakati wa mavuno na mauzo ya mazao yao.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Beasley alikutana Rais Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo aliahidi kuongeza ununuzi wa mazao ya chakula kwa wakulima ikiwemo mahindi ili kuondoa tatizo la ununuzi wa mazao yao.
Katika mazungumzo yake na Rais Magufuli, Beasley alisema WFP imepanga kununua jumla ya tani 31,000 za mahindi yanayolimwa nchini na kuyapeleka katika nchi za Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Somalia sehemu mbalimbali duniani zinazokabiliwa na njaa.
Aidha kabla ya Bw. Beasley kukutana na Rais Magufuli, tayari tangu mwaka 2016 WFP tayari wametiliana saini katika hati ya makubaliano na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika kwa ajili ya kuuziana nafaka mbalimbali, ikiwemo zao la mahindi.
Anaongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, WFP tayari imenunua kiasi cha tani 200,000 kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoa misaada ya kibinadamu katika maeneo ya na ndani nje ya nchi.
Shirika la WFP linafanya kazi katika nchi 80 Duniani ambapo katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania inatajwa kuwa ndiyo nchi pekee yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha nafaka, ambapo mwaka 2017 shirika hilo lilinunua tani 80,000 hadi 100,000 hapa nchini zenye thamani ya Dola Milioni 18.
Ushirikiano wa NFRA na WFP ni kiashiria cha matumaini mpya kwa wakulima wadogo na wakubwa nchini, Serikali kwa upande wake imebuni imebuni mikakati mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini kama vile Kagera, Mwanza, Shinyanga, Singida, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, ambapo vingi kati ya viwanda hivyo vinatumia malighafi za kilimo.
Uzinduzi wa viwanda hivyo vinatarajia kuelta muunganiko wa shughuli za viwanda na kilimo nchini, jambo ambalo lilishindikana kwa muda mrefu, hivyo ni wajibu wa wakulima kutumia bora za kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

No comments

Powered by Blogger.